Picha ya dhana ya Nuhu kando ya Safina
← Hadithi ya Nuhu

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (2015)

Safina ya Nuhu katika Biblia:
Maandiko ya Mwanzo 6–9

Soma masimulizi kamili ya Biblia ya Safina ya Nuhu na Gharika katika Mwanzo sura ya 6 hadi 9 mstari kwa mstari kwa usomaji wa familia na masomo ya shule ya Jumapili.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (2015) — ebible.org.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ / The Holy Bible in Swahili, Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc.; translated by Biblica, Inc.; Kiswahili (Swahili). Source: eBible.org.

Credit the copyright holder and source, indicate changes without implying endorsement, and share adaptations under the same license. See the source copyright notice.

CC BY-SA 4.0

Mwanzo · Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (2015)

Sura 6

  1. Watu walipoanza kuongezeka idadi katika uso wa dunia na watoto wa kike wakazaliwa kwao,
  2. wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa yeyote miongoni mwao waliyemchagua.
  3. Ndipo Bwana akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa, siku zake zitakuwa miaka 120.”
  4. Wanefili walikuwako duniani siku hizo, na baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa na watu waliojulikana wa zamani hizo.
  5. Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu.
  6. Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko.
  7. Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”
  8. Lakini Noa akapata kibali machoni pa Bwana.
  9. Hivi ndivyo vizazi vya Noa. Noa alikuwa mtu wa haki, na mkamilifu miongoni mwa watu wa wakati wake, tena alitembea na Mungu.
  10. Noa alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi.
  11. Wakati huu dunia ilikuwa imejaa uharibifu na ukatili machoni pa Mungu.
  12. Mungu akaona jinsi dunia ilivyoharibika, kwa maana watu wote duniani walikuwa wameharibu njia zao.
  13. Kwa hiyo Mungu akamwambia Noa, “Nitawaangamiza watu wote, kwa kuwa dunia imejaa ukatili kwa sababu yao. Hakika mimi nitaangamiza watu pamoja na dunia.
  14. Kwa hiyo jitengenezee safina kubwa kwa mbao za mvinje, tengeneza vyumba ndani yake na uipake lami ndani na nje.
  15. Hivi ndivyo utakavyoitengeneza: Safina iwe na urefu wa dhiraa 300, upana wake dhiraa hamsini na kimo chake dhiraa thelathini.
  16. Itengenezee paa na umalizie safina kwa kuacha nafasi ya dhiraa moja juu. Weka mlango ubavuni mwa safina, na uifanye ya ghorofa ya chini, ya kati na ya juu.
  17. Nitaleta gharika ya maji juu ya nchi ili kuangamiza uhai wote chini ya mbingu, kila kiumbe chenye pumzi ya uhai ndani yake. Kila kitu juu ya nchi kitaangamia.
  18. Lakini Mimi nitaweka Agano langu na wewe, nawe utaingia ndani ya Safina, wewe pamoja na mke wako, wanao na wake zao.
  19. Utaingiza ndani ya Safina kila aina ya kiumbe hai wawili wawili, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja na wewe.
  20. Wawili wa kila aina ya ndege, wa kila aina ya mnyama na wa kila aina ya kitambaacho ardhini watakuja kwako ili wahifadhiwe hai.
  21. Utachukua kila aina ya chakula kitakacholiwa, na ukiweke akiba kama chakula kwa ajili yako na yao.”
  22. Noa akafanya kila kitu kama vile Mungu alivyomwamuru.

Mwanzo · Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (2015)

Sura 7

  1. Ndipo Bwana akamwambia Noa, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.
  2. Uchukue wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi wa kiume na wa kike.
  3. Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote.
  4. Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya nchi kwa siku arobaini usiku na mchana, nami nitafutilia mbali kutoka uso wa nchi kila kiumbe hai nilichokiumba.”
  5. Noa akafanya yote kama Bwana alivyomwamuru.
  6. Noa alikuwa na miaka 600 gharika ilipokuja juu ya dunia.
  7. Noa na mkewe na wanawe na wake zao wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika.
  8. Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vitambaavyo,
  9. wa kiume na wa kike, walikuja kwa Noa wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Noa.
  10. Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia.
  11. Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili mwaka wa 600 wa kuishi kwake Noa, siku hiyo ndipo chemchemi zote hata zilizo chini sana ya ardhi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa.
  12. Mvua ikanyesha juu ya nchi siku arobaini usiku na mchana.
  13. Siku hiyo Noa, na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao wakaingia katika ile safina.
  14. Nao walikuwa pamoja na kila mnyama wa mwituni kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa.
  15. Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai ndani yake vikaja kwa Noa viwili viwili, vikaingia katika safina.
  16. Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Noa, ndipo Bwana akamfungia ndani.
  17. Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi.
  18. Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji.
  19. Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote.
  20. Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano.
  21. Kila kiumbe hai kitambaacho juu ya nchi kikaangamia: Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi na wanadamu wote.
  22. Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa.
  23. Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Noa peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
  24. Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.

Mwanzo · Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (2015)

Sura 8

  1. Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa naye ndani ya safina, akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakaondoka.
  2. Zile chemchemi zilizo chini sana ya ardhi pamoja na malango ya mafuriko ya mbinguni yakawa yamefungwa nayo mvua ikawa imekoma kunyesha kutoka angani.
  3. Maji yakaendelea kupungua taratibu katika nchi. Kunako mwisho wa siku ya 150, maji yalikuwa yamepungua,
  4. katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati.
  5. Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
  6. Baada ya siku arobaini Noa akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina
  7. na akamtoa kunguru, akawa akiruka kwenda na kurudi mpaka maji yalipokwisha kukauka juu ya nchi.
  8. Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya uso wa ardhi.
  9. Lakini hua hakupata mahali pa kutua kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Noa ndani ya safina. Noa akanyoosha mkono akamchukua yule hua akamrudisha ndani ya safina.
  10. Noa akangojea siku saba zaidi kisha akamtoa tena hua kutoka safina.
  11. Wakati hua aliporejea kwa Noa jioni, alikuwa amechukua katika mdomo wake jani bichi la mzeituni, lililochumwa wakati ule ule! Ndipo Noa akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya uso wa dunia.
  12. Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Noa.
  13. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Noa, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Noa akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka.
  14. Katika siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili dunia ilikuwa imekauka kabisa.
  15. Ndipo Mungu akamwambia Noa,
  16. “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao.
  17. Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
  18. Kwa hiyo Noa akatoka nje pamoja na mkewe, wanawe na wake zao.
  19. Wanyama wote na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi na ndege wote, kila kitu kiendacho juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina, kila aina ya kiumbe, kimoja baada ya kingine.
  20. Kisha Noa akamjengea Bwana madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.
  21. Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.
  22. “Kwa muda dunia idumupo, wakati wa kupanda na wa kuvuna, wakati wa baridi na wa joto, wakati wa kiangazi na wa masika, usiku na mchana kamwe havitakoma.”

Mwanzo · Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (2015)

Sura 9

  1. Ndipo Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia.
  2. Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu.
  3. Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.
  4. “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai.
  5. Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.
  6. “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu, kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimuumba mwanadamu.
  7. Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.”
  8. Ndipo Mungu akamwambia Noa na wanawe pamoja naye:
  9. “Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu,
  10. pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani.
  11. Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.”
  12. Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo:
  13. Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia.
  14. Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni,
  15. nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote.
  16. Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
  17. Hivyo Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”
  18. Wana wa Noa waliotoka ndani ya safina ni: Shemu, Hamu na Yafethi. (Hamu ndiye alikuwa baba wa Kanaani.)
  19. Hawa ndio waliokuwa wana watatu wa Noa, kutokana nao watu walienea katika dunia.
  20. Noa akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu.
  21. Alipokunywa huo mvinyo wake akalewa na akalala uchi kwenye hema lake.
  22. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.
  23. Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.
  24. Noa alipolevuka kutoka kwenye mvinyo wake na kujua lile ambalo mwanawe mdogo kuliko wote alilokuwa amemtendea,
  25. akasema, “Alaaniwe Kanaani! Atakuwa mtumwa wa chini sana kuliko watumwa wote kwa ndugu zake.”
  26. Pia akasema, “Abarikiwe Bwana, Mungu wa Shemu! Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.
  27. Mungu na apanue mipaka ya Yafethi; Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu, na Kanaani na awe mtumwa wake.”
  28. Baada ya gharika Noa aliishi miaka 350.
  29. Noa alikuwa na jumla ya miaka 950, ndipo akafa.

Usomaji uliounganishwa

Paka rangi na uchunguze pamoja na Mwanzo 6–9

Linganisha kila sura unayosoma na kurasa 100 za kuchora za A4 kwa mpangilio, karatasi 8 za familia ya Nuhu na mifano ya 3D.